Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Tanzania, Jaji Frederick Werema amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia
jana, Jumanne, kufuatia sakata la uchotaji wa fedha kutoka akaunti ya
ESCROW ambapo zaidi ya dola milioni 120 zilihamishwa.
Mwanasheria
mkuu, pamoja na baadhi ya wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali
walituhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika
kwa miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta.
|
Mwanasheria mkuu wa serikali Jaji Frediriki Welema |
Leonard Mubali ameandaa taarifa ifuatayo:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya
Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu huyo wa
Serikali.
Katika barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema amesema
ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti
ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua hali ya hewa. Rais Kikwete
amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na
uadilifu.
kamati ya Bunge ya hesabu za Serikali ilipeleka pendekezo kumtaka Jaji Werema kuwajibika
Sakata la Akaunti ya Escrow
liliibuliwa bungeni na mmoja wa wabunge wa bunge la Tanzania, David
Kafulila na kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.
|
Kamati ya Bunge ya hesabu za serikali ilipeleka mapendekezo ya kumtaka Jaji Welema awajibike |
Baada
ya uchunguzi kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni
mwa mwezi Novemba, kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu
taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika
akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni
mwa maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu,
maafisa waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma,
viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika
katika kashfa hii na hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia
hatua za kisheria wahusika na wengine kuondolewa katika nyadhifa zao za
kuteuliwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Zitto Kabwe
Kamati hiyo ya Bunge pia
ilipendekeza kuwa waziri wa Nishati na Madini, waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, mwanasheria mkuu, katibu mkuu wa wizara ya
Nishati na Madini na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Tanesco
wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
|
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya hesabu za serikali Zitto Kabwe |
Pia
maazimio ya Kamati ya kudumu ya bunge ilipendekeza kuwa, kwa miaka
mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na makampuni
binafsi imeisababishia Tanesco hasara ya mabilioni ya fedha na kutishia
uhai wake wa kifedha, serikali iwasilishe mikataba husika bungeni au
kwenye kamati zake kwa lengo la kutekeleza vema wajibu wake wa kuimamia
na kuishauri serikali.
Akaunti ya Escrow ilianzishwa katika Benki
Kuu ya Tanzania ili kuhifadhi fedha, baada ya kuibuka kwa mvutano kati
ya Shirika la Umeme la Tanzania, Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya
IPTL kuhusu ongezeko la mtaji wa uwekezaji, huku TANESCO ikilalamika
kuwa gharama za kununua umeme kutoka kampuni ya IPTL zilikuwa za juu
mno. Fedha hizo zingeendelea kutunzwa katika Akaunti hayo hadi wakati
ambapo suluhisho la mvutano wa wabia hao wawili lingepatikana.